Pages

Subscribe:

Monday, December 25, 2017

EMANUEL EBOUE ATAKA KUJIUA PIA ATAJA SABABU ZA KUTO PATA MSAADA

Tunaelekea msimu wa sikukuu za Xmass na mwaka mpya na dunia nzima iko na mihangaiko kuelekea siku hizi kubwa za mwaka, lakini hali kwa kiungo wa zamani wa Arsenal na timu ya taifa ya Ivory Coast Emmanuel Eboue ni tofauti kabisa.

Taarifa zinasema Eboue anataka kufanga jaribio la kujiua kutokana na hali mbaya inayomkabili katika maisha yake, ripoti zinasema kiungo huyo ameyumba sana kiuchumi kiasi cha kuona...
uhai hauna thamani tena kwake.

Eboue alikuwa akipokea kiasi kikubwa katika klabu ya Arsenal huku akipokea zaidi ya £1.5m wakati akiichezea klabu ya Galatasaray lakini inasemekana kwamba talaka na mkewe huenda ikakomba kila kitu alichonacho.

Talaka kati ya Eboue na mkewe aliyetambulika kwa jina la Aurellie imemfanya Eboue kuwa na msongo wa mawazo mkubwa unaochangiwa na kuzuiliwa kuwatembelea watoto wake watatu Mathis, Clara na Maeva katika msimu huu wa Xmass.


Inafahamika kwamba Eboue alimpa mamlaka na haki ya kumiliki mali zote walizokuwa nazo na kitendo ya kutalakiana kinamaanisha Eboue atapoteza kila kitu alichomuandikishia mwanamke huyo baada ya kushindwa kesi ya talaka mahakamani.

Achana na majanga hayo ya Eboue lakini mchezaji huyo alitoka kufiwa na babu yake nchini Ivory Coast aliyefariki kwa kansa huku kaka yake aliyefahamika kwa jina la N’Dri Serge naye alifariki kwa ajali ya pikipiki.

Matatizo ya Eboue ya umiliki wa baadhi ya vitu ikiwemo nyumba yake ya kisasa iliyoko London  na hana pesa ya kuwalipa watetezi wa kisheria hali ambayo inakaribia kupelekea baadhi ya nyumba na mali alizobakiwa nazo kuuzwa.

“Naogopa hata watu kufahamu kwamba niko ndani, sina amani nikiwa ndani maana nawaza muda wowote polisi wanaweza kuja kuniondoa, siwashi hata taa maana sitaki watu nje wajue kwamba nipo” alisema Eboue.

Mbaya zaidi Eboue amesema amekuwa na mawazo ya kujiua kwa sasa kutokana na hali ilivyobadilika katika maisha yake na amekuwa akimuomba mungu sana amuondolee mawazo hayo mabaya kichwani mwake.

Akielezea kwa majonzi makubwa sana Eboue anakumbuka namna alivyotoka katika mazingira magumu hadi kupata pesa na kisha kununua nyumba lakini sasa hana amani katika nyumba yake mwenyewe.

Eboue analala katika nyumba ya rafiki yake ambapo inasemekana analala chini huku hana hata pesa ya kupelekea nguo dry cleaner hali inayompelekea kutumia mikono yake kufua nguo.

Eboue anasikitisha sana na amesema anatamani klabu yake ya zamani ya Arsenal imsaidie katika kipindi hiki kigumu lakini atajisikia vibaya kama akionana na wachezaji wenzake wa zamani akiwemo Thiery Henry.

Dunia imeshtushwa sana na habari za kiungo wa zamani wa Arsenal na timu ya taifa ya Ivory Coast, wengi wamekuwa wakihoji inakuwaje nyota mkubwa kama huyo ambaye amewahi kuwa tajiri mkubwa kuanguka kiuchumi.

Inafahamika kwamba Emmanuel Eboue wakati akicheza soka lazima alikuwa na marafiki wakubwa ambao walikuwa na uwezo mkubwa sana kifedha ikiwemo wachezaji na hata kocha wa Arsenal Arsene Wenger, kwa nini hawamsaidii?

“Wakati wa matatizo haya yakiendelea nilipoteza simu yangu ambayo kulikuwa na namba nyingi, Wenger tulikuwa tukiongea lakini tangu nipoteze simu sijawahi kuwasiliana naye pamoja na marafiki zangu” anasema Eboue.

Eboue anasisitiza kwamba kwa sasa anapokea msaada kutoka kwa mtu yeyote lakini kama vilabu ambavyo alikuwa akivitumikia awali Galatasaray au Arsenal wataamua kumsaidia baasi atafurahi sana.

Eboue anasema ana ndoto za kurudi Arsenal kuwasaidia wachezaji wadogo na kwa sasa hataki kazi kubwa sana kwani hata kazi ndogo tu itakayompatia kipato kidogo itakuwa muhimu sana kwake katika kipindi hiki.

Eboue anasema anataka kuendelea kucheza soka lakini pia akasema ataona aibu kama akipewa kazi ya kuwafundisha vijana wa Arsenal halafu akakutana na wachezaji ambao zamani alicheza nao ataona aibu.

Mashabiki mtandaoni wameibuka na wakimpa pole kwa lililompata na huku wengine wakienda mbali kwa kuiomba klabu ya Arsenal kutoa msaada kwa kiungo wao huyo wa zamani.

Pamoja na yote na pia ni somo kwa vijana wa Kiafrika lakini Emmanuel Eboue haachi kumshukuru Mungu na amesema yote yanayoendelea katika maisha yake ni mpango wa mungu na hatamani yamtokee mtu mwingine.

0 comments:

Post a Comment