ILIPOISHIA JANA…
“Karibu mpaka ndani bwana mdogo,” mzee alinikaribisha. Nami nikajimwaga katika kiti kimoja cha mbao, huku nikiliacha jicho liichunguze nyumba ile.
INAENDELEA
Ilikuwa ni nyumba yenye vyumba vitatu na sebule. Kila kitu kilikaa hovyohovyo hata panya na popo walikuwa ni miongoni mwa wakazi wa nyumba hiyo. Ukimwondoa mzee, popo na...
wale panya, wakazi wengine niliowashuhudia walikuwa: nzi, mende, kunguni, chawa, viroboto, mbu na mijusi wakubwa waliotukana matusi kwa kutikisa vichwa!
“Haya eleza kisa cha kunifuata mpaka katika nyumba hii waiogopayo watu!” mzee alichokoza mada, akiwa naye kakaa juu ya kiti cha mbao kama nilichokalia. Tukawa tukitazamana kwa jicho la pembeni.
“Mzee nashukuru kwa nafasi hii! Nina matatizo mzee wangu, nisamehe kwa makosa niliyofanya… mtu wako wa ajabu hunifukuza siku zote mpaka maisha yangu yamebadilika, nashindwa hata kufanya kazi! Nisamehe kwa makosa niliyofanya na naomba uniondolee adhabu hii.”
“Heh! Inaonekana una matatizo sana kijana… kwanza tumekosea, bado hatujapata kufahamiana. Vipi kijana, una jina?”
“Jina ninalo, naitwa Mako, ila jina langu maarufu ni Popo!”
“Popo!” alishangaa mzee, “kwa nini uitwe Popo na wewe ni binadamu?”
“Uhuni na starehe mzee wangu ndiyo zilinipa jina hilo.”
Na ndizo zilizosababisha mpaka sasa uko na mimi hapa.”
“Swadakta mzee, nisaidie, kamba ngumu!”
“Nikusaidie nini? Unataka kuacha uhuni na starehe? Lakini mimi si mganga.”
“Hapana mzee! Nafukuzwa na mtu wa ajabu siku zote… mzuie mtu wako, atanimaliza!”
“Ha ha haaaaah!” mzee alicheka, “Unamaanisha ulifanya uzinzi juu ya kaburi la mjukuu wangu Chimota!”
“Ndiyo mzee, nisamehe ni ujana tu!”
“Huyo anayekufukuza hana uwezo wa kukutoa uhai… ooh nimetoa siri.”
“Hilo nalijua mzee, lakini kitendo cha kukimbizwa na kutishwatishwa kinaudhi kuliko kifo.” “Hukijui kifo… kwa sababu umenipata nitakusaidia, nenda nyumbani kesho njoo tufanye mkakati wa kumsimamisha mtu wa ajabu kama usemavyo.”
Sikukubali kuondoka mahali pale bila kupatiwa tiba ya tatizo lililonisumbua. Nikamwomba mzee nilale kwake. Hakuwa mtu wa maneno mengi, alikubali.
“Nyumba hii haijawahi kulala mtu mwingine zaidi yangu kwa miaka mingi sasa!” alisema mzee akinipeleka chumbani.
“Kwa sababu gani?”
“Ulozi!” alijibu mzee, nikapata hofu ya kulala ndani ya nyumba yake. "Itakuwaje kama akinitoa kafara kwa wachawi wenzake?" niliwaza.
Popo atalala ndani ya nyumba? Akikubali kuondoka atampata tena mzee?
Tukutane kesho..



Follow on Instagram
0 comments:
Post a Comment