Pages

Subscribe:

Wednesday, April 5, 2017

STORY: FUTA MACHOZI MPENZI 01

 
“Unafanya nini hapo binti?” ilisikika sauti ya mwanaume mmoja kutoka katika gari la kifahari, lilikuwa Range Rover SUV ya rangi ya kijivu yenye gharama zaidi ya milioni mia moja. “Nasubiri usafiri!” alijibu msichana huyo aliyeulizwa swali, sauti yake ilikuwa nyororo mno, alivaa sketi fupi na laini iliyoyaacha mapaja yake wazi kwa asilimia kubwa.

“Unauza tuongee biashara?” aliuliza mwanaume huyo.
“Nani? Mimi? Hapana! Nimetoka kwenye pati,” alijibu msichana huyo huku akionekana...

kushtuka, hakuamini kama angeulizwa swali kama hilo, ila hakukasirika kwani mavazi yake yalionyesha kama msichana aliyekuwa akijiuza.

“Sawa. Unaishi wapi?”
“Manzese Midizini!”
“Naweza kukusaidia kukupa lifti?”
“Mmh! Hapana baba! Wewe endelea na safari yako,” alisema msichana huyo huku akionekana kuwa na hofu kubwa.


“Wala usijali! Mimi si mtu mbaya, ni mtu mwema, si unaona natembea na Biblia, wala usihofu,” alisema mwanaume huyo huku akiitoa Biblia na kumuonyeshea msichana huyo ambaye kidogo akaonekana kuwa huru.
Msichana huyo alikuwa amesubiri usafiri kwa kipindi kirefu hapo barabarani, alihitaji lifti na usiku huo alikuwa akitoka katika sherehe ya kuzaliwa ya rafiki yake aliyeitwa Zaituni. Huko, hakuwa na raha, kila mwanaume alikuwa akimwangalia yeye, alivalia nguo nyepesi ambayo iliyafanya maungo yake kuonekana vizuri kabisa.


Alikosa amani, hata alipokuwa akitembea, macho yake yalikuwa huku na kule, aliogopa, hakuwa na amani kabisa mpaka alipoamua kuondoka katika sherehe hiyo. Aliondoka kisiri, hakutaka mwanaume yeyote yule amuone kwani aliogopa kufuatiliwa, hilo akafanikiwa na kufika mpaka barabarani. 


Hakujua ni kwa namna gani angeweza kurudi nyumbani kwao, hakuwa na fedha, hakuwa na usafiri wowote ule, aliogopa na pale alipokuwa moyo wake ulikuwa na hofu ya kubakwa, alihisi muda wowote ule wanaume wangetokea na kumbaka.
Kwa sababu Kinondoni ilikuwa sehemu moja iliyokuwa na machangudoa wengi, walipomuona, walihisi kwamba alikuwa mwenzao hivyo hawakutaka kujali sana. Akaondoka mpaka alipofika barabarani, alijitenga na kusimama pembeni kabisa, tena akiwa peke yake.


Watu waliokuwa wakipita na magari, waliyasimamisha na kushusha vioo, walimwangalia msichana huyo kwa macho yaliyojaa matamanio, walitamani kumpandisha ndani ya gari na kuondoka naye lakini maneno yao yote yalionyesha kuwa walitaka kulinunua penzi lake kwani kwa jinsi alivyoonekana, alikuwa na mvuto wa ajabu.


“Twende binti! Nina laki moja hapa, haina matumizi yoyote yale,” alisema jamaa mmoja aliyekuwa ndani ya gari yake.
“Hapana! Wewe nenda tu!”
“Jamaniiiiiii!”
“Nimesema nenda tu kaka yangu,” alisema msichana huyo.
Alikaa hapo mpaka ilipofika saa nane usiku. Mwili wake ulikuwa ukitetemeka, mbali na baridi alilokuwa akilihisi lakini bado hofu kubwa iliutawala moyo wake na kumfanya kutokwa na kijasho chembamba kwa mbali. 


Alimuomba Mungu usiku huo uwe na amani kwani pale aliposimama, hakukuwa na mtu yeyote aliyekuwa akipita, ni magari tu ndiyo yaliyokuwa yakimpita na mengine kumpigia honi mpaka alipokuja huyo mzee ambaye akamchukua na kuondoka naye.
“Unaitwa nani binti?” aliuliza mzee huyo kwa sauti ya utaratibu.
“Pamela Ndanshau!”
“Ooh! Sawa. Mimi naitwa Edward,” alijitambulisha mzee huyo.


“Sawa. Nimefurahi kukufahamu baba!”
“Mimi si mkubwa, ni kijana tu Pamela, unaweza kuniita rafiki au mshikaji wa mjini,” alisema mzee huyo huku akiachia tabasamu, japokuwa kichwa chake kilikuwa na mvi nyingi lakini aliukataa ukubwa, kwake, alijiona kuwa kijana wa miaka ishirini.
Walikuwa wakizungumza mengi, mzee Edward alikuwa mchangamfu, kila wakati yeye ndiye aliyekuwa akitawala mazungumzo ya humo garini. Moyo wake ulifurahi mno, kitendo cha kukutana na msichana mrembo kama alivyokuwa Pamela, kwake ilikuwa ni bahati kubwa.


Pamoja na kuongeea kwa uchangamfu, bado macho yake hayakutulia, kila wakati alikuwa akiangalia mapaja ya msichana huyo, yalinona, yalimtamanisha mno, kila alipomwangalia pepo la ngono lilimuingia na kumtoka, likamuingia tena na kumtoka.
“Mmh! Anatamanisha! Mtoto amenona sana! Hivi kwa nini nilizaliwa zamani? Nilitakiwa kipindi kama hiki kuwa kijana,” alijisemea Mzee Edward huku akiendelea kuyaangalia mapaja ya Pamela kisiri.


Pamela hakuwa na amani, kichwa chake kilikuwa na mawazo, japokuwa mzee huyo alijifanya kuwa mcha Mungu kwa kumuonyeshea Biblia lakini bado hakuwa na amani, alimwangalia, macho yake yalionyesha tamaa kubwa, wakati mwingine alitamani kuteremka na kutembea lakini ilishindikana kabisa.


Mzee Edward hakuongea naye mambo ya mapenzi, alimuonyeshea wema mkubwa wa kumsaidia kwani pale alipokuwa amesimama, haikuwa sehemu salama, moyo wake ulimwambia ni lazima amsaidie msichana huyo mrembo.


Hawakuchukua muda mwingi wakafika Manzese Midizini, mzee huyo akasimamisha gari mbele ya nyumba moja iliyoonekana kawaida sana, hakukuwa na mtu, kulikuwa na ukimya mkubwa mahali hapo, Pamela akamshukuru Mzee Edward na kisha kuufungua mlango wa gari kwa ajili ya kuteremka.


“Pamela...” aliita mzee huyo, Pamela akamgeukia.
“Abeee...”
“U msichana mzuri sana, hukutakiwa kuwa mahali pale, tena kwa wakati kama huu, unaishi na nani hapa?” aliuliza mzee huyo.
“Mama na mdogo wangu!”
“Sawa. Nitakuja kukuona kesho! Una simu?”
“Ndiyo!”
“Naruhusiwa kuwa na namba yako?”
 

Kabla ya kujibu chochote, Pamela akanyamaza na kuangalia chini, alionekana kuwa na hofu. Mzee huyo hakuonekana kama alikuwa mtu mbaya na ndiyo maana tangu alipomsaidia mpaka wanafika hapo, hakumwambia neno lolote la kimapenzi, alimsaidia kama mtu aliyekuwa akihitaji msaada mkubwa.

Hakuona kama ulikuwa uungwana wa kumnyima namba mzee huyo kwani bila wema wake, inawezekana bado angeendelea kuwa kule barabarani akisubiri lifti kutoka kwa watu wengine, je, ingekuwaje kama angepewa lifti na mwanaume ambaye angemtaka kimapenzi kinguvu?


“Hii hapa! Andika,” alisema Pamela na kisha kumtajia namba ya simu Mzee Edward, alipoiandika, akachukua bahasha na kumpa Pamela, kwa jinsi bahasha ile ilivyoonekana, ilionyesha ndani kulikuwa na kitu, hakujua kulikuwa na nini ila akahisi kwamba zilikuwa pesa, alipoipokea, akateremka.


Mzee Edward hakutaka kuondoka mahali hapo mpaka pale ambapo angehakikisha Pamela ameingia ndani. Alibaki mahali hapo, Pamela akaanza kugonga mlango, baada ya dakika chache, kijana mmoja akaufungua mlango na kuingia ndani.


“Bye...” alisema Mzee Edward kwa sauti, Pamela hakuitikia zaidi ya kumpungia mkono kumuaga. Mzee Edward akawasha gari na kuondoka zake huku akionekana kuwa mwenye furaha tele kukutana na msichana huyo.

Je, nini kitaendelea?
Je, msichana huyo ataweza kuwa na Mzee Edward?
Nini kitatokea baadaye?
Tukutane Jumanne mahali hapahapa.
Unaweza kushare kwa marafiki zako pia.


******************** ************************ ************************* ********************
Simulizi zitakujia hapa hapa kila siku kuanzia saa tatu asubuhi mpaka saa nne asubuhi na ukipitwa na story basi nenda hapo juu kwenye menyu kisha bofya mahali palipo andikwa LOVE & STORY. Pia waweza kudownload Application yetu kwa kubofya neno DOWNLOAD hapo chini ufuate na maelekezo ili uweze kupata story na updates mbalimbali kwa muda muafaka na kwa urahisi zaidi.
 

Tukutane tena kesho muda kama huu.. ahsante


Download

0 comments:

Post a Comment